Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Fakharia
Khamis amehoji bungeni adhabu gani askari anapewa ikiwa atashindwa kutoa
saluti kwa mbunge.Katika swali la nyongeza mbunge huyo alitaka kujua
maana ya saluti kwa askari ni nini, na viongozi gani wa uraiani
wanaotakiwa kupigiwa saluti katika mhimili wa Bunge, Serikali na
Mahakama.Akijibu swali la mbunge huyo, Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na
Uvuvi, William Ole Nasha kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi
alisema Serikali imetangaza adhabu ya kuwakata mishahara na adhabu
nyingine, askari polisi wote nchini ambao hawatawapigia saluti wabunge
wa Bunge la Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Ole Nasha alisema kumpigia saluti mbunge
ni jambo la lazima kwa askari kwa kuwa lipo kwenye moja ya masharti
yao, hivyo kutokufanya hivyo ni kushindwa kutii kiapo cha uaminifu wao.
“Askari asipotoa saluti unatakiwa kumripoti kwa kiongozi wake ambapo
atapewa adhabu ikiwamo kukatwa mshahara, kupigishwa paredi, kufanya
usafi katika maeneo ya vituo na adhabu nyingine nyingi zinazofanana na
hizo,” alisema Ole Nasha. Alisema saluti ni salamu ya kijeshi ambayo
hutolewa na askari kwa mujibu wa kanuni za kudumu za utendaji za jeshi
la polisi (Police General Orders –PGO No 102).
Naibu Waziri alisema sheria hiyo
imewataja askari wa vyeo vyote kuwa wanatakiwa kupiga saluti kwa Rais wa
Jamhuri na Rais wa Zanzibar, Makamu wa Rais na Makamu wawili wote wa
Zanzibar, majaji wakuu wa Muungano na Zanzibar.Wengine ni Spika wa
Muungano na Zanzibar, mawaziri wote wa Jamhuri na Zanzibar, makatibu wa
Bunge na Baraza la Wawakilishi, wabunge wa muungano na wawakilishi
wanapokuwa kwenye maeneo yao, wakuu wa mikoa, majaji wanapokuwa kwenye
maeneo yao na kwa nafasi zingine ni wakuu wa wilaya na mahakimu kwenye
maeneo yao.
Post a Comment